Shirika la Anga za Juu la Iran limetangaza mipango mikubwa ya mwaka 2026, ikiwemo kuzindua satelaiti ya kwanza ya rada iliyotengenezwa nchini, kuendeleza mradi wa satelaiti 24 za “Shahid Soleimani” na kuharakisha maendeleo ya satelaiti za mawasiliano na uchunguzi wa ardhini.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, Mkuu wa Shirika la Anga za Juu la Iran, Hassan Salarieh, ametangaza mpango kabambe wa maendeleo ya sekta ya anga za juu kwa mwaka 2026, ukijumuisha uzinduzi wa satelaiti ya kwanza ya rada iliyobuniwa na kutengenezwa nchini pamoja na kuendeleza mfumo wa satelaiti wa “Shahid Soleimani” wenye jumla ya satelaiti 24.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Salarieh alisema kuwa miradi ya anga za juu inayotekelezwa kwa sasa inahusisha ujenzi wa miundombinu, utengenezaji wa satelaiti na huduma zinazotegemea taarifa na picha kutoka angani. Alieleza kuwa Iran imepiga hatua kubwa katika kuimarisha vituo vya kudhibiti satelaiti, maabara za anga za juu na kituo cha kurushia makombora ya anga kilichopo Chabahar.
Aliongeza kuwa satelaiti ya mawasiliano Nahid-3 ipo katika hatua ya usanifu na utengenezaji wa mifumo yake, baada ya mafanikio ya satelaiti ya Nahid-2 iliyozinduliwa mwaka uliopita.
Kuhusu mfumo wa “Shahid Soleimani”, Salarieh alisema awamu ya kwanza itajumuisha satelaiti 24, zikiwemo 18 za msingi na 6 za akiba. Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu ili kutoa huduma za mawasiliano ya data katika maeneo ya dharura na sehemu zisizo na miundombinu ya mawasiliano ya ardhini, huku ukiwa na teknolojia ya mawasiliano kati ya satelaiti (ISL).
Aidha, alitangaza kuwa satelaiti ya rada ya kwanza ya Iran, Rad-1, itazinduliwa hivi karibuni baada ya kucheleweshwa kwa sababu za kiufundi, huku maendeleo ya satelaiti yenye uwezo mkubwa zaidi, Rad-2, yakiendelea katika Taasisi ya Anga za Juu ya Iran.
Salarieh pia alisema Iran inaendelea kuboresha satelaiti za uchunguzi wa ardhini, ikiwemo Pars-2 inayosubiri kuzinduliwa na Pars-3 inayoundwa kwa uwezo wa kutoa picha zenye usahihi wa mita moja. Alisisitiza kuwa kufikia mzunguko wa kudumu wa satelaiti (GEO) katika urefu wa kilomita 36,000 ni moja ya vipaumbele muhimu vya kimkakati vya sekta ya anga za juu nchini humo.
Maoni yako